![](https://blogger.googleusercontent.com/img/a/AVvXsEiT9jlemK1NSJivGg584McFC6Rlx3OeTlHzjLWbEJgFA4s9a7anWzfxCbA17Zxrppu-ez2qhQ4IFVE6HqzVqEEBNXnEbD2gEYIW2J2psPDB2v8EHkK_Gwwh2gG-MY0e04Dfs49w4yuZFUJ_WxkcTwPSEq9DPyKZs3gQHSBLgtujq9OZLplRUegXangV=w640-h360)
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/a/AVvXsEhkRgz9GRm-xsV9vriuUyAUkxfCVL6rLHGZVQ8_Nb0abNpfIKCTZFVHZFqAb7mdyhoqdqnhQP2kYkesbi8ZD43oKISG2DudyjIKaIG8vMCPKKZUbyfbVgFCT00oUAbi83Rm6K4XTGNpFCJwpKYFGFECIB-__2m3i2FYoY8KgaErE_jmT97WiRxPtA88=w640-h360)
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mpanda,Mhe.Haidary Sumry akizungumza na wanakikundi cha Watu wenye ulemavu (Tujiendeleze).
********************************************************
"Mkopo tuliopata kutoka Halmashauri, umetuwezesha kupunguza ukali wa maisha ambapo kwasasa familia zetu zina uwezo wa kula Milo mitatu kwa siku ukilinganisha na hapo awali"
Na.Swaum Katambo
Mpanda-Katavi
Ni wajibu uliowekwa na sheria kwa Serikali za Mitaa kutenga asilimia kumi ya mapato yanayokusanywa kutoka kwenye vyanzo vya ndani vya mapato kwa ajili ya kutoa mikopo kwa vikundi vilivyosajiliwa vya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu.
Mwongozo huu unaelezea kwa lugha nyepesi kanuni zilizowekwa chini ya sheria ya fedha ya serikali za mitaa chini ya kifungu cha 37 ambazo zinajulikana kama kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu za mwaka 2019 ambazo zinatumika katika Mamlaka zote za Serikali za Mitaa Tanzania Bara.
Kikundi cha watu wenye ulemavu Tujiendeleze kilichopo Kijiji cha Dirifu Manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi ni moja ya wanufaika wa 10% ya Mapato hayo ambapo kwa upande wa watu wenye ulemavu hunufaika na 2% kati ya 10% zinazotolewa.
Kikundi hicho kinachojishughulisha na shughuli za uchenjuaji wa dhahabu kiliwezeshwa Mashine ya Kusaga Mawe ya Dhahabu (Crusher) yenye thamani ya Tsh Mil 10.
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/a/AVvXsEhNNTVtCS9VQNJlotcc-kCLkHIloGHl9OPesvgFNJH_OqGaDtwZsSsEMc9GJVxXwN3983S661QvPNhFjY09QL-eUKu9rcmt2WUjYQy61T_zzriVaEAZAC2ODqkKZEs-ElzMn2J27qm6pwQeQxJllhJFJH4X7UZrOtrMJmcCs-QZhU9SiaF3BJtcjNDy=w640-h360)
Wanakikundi hao wamesema kuwa Mkopo waliopata kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda umewawezesha kupunguza ukali wa maisha ambapo kwasasa familia zao wana uwezo wa kula Milo mitatu kwa siku ukilinganisha na hapo awali walipokuwa wakishindia mlo mmoja au miwili kabla ya kugundua fursa ya Mikopo hiyo.
Bwana Joshua Mnoga alisema Baada ya kupata mashine ya kusaga dhahabu (Crusher) si tuu kuwarahisishia katika utendaji kazi lakini pia wameendelea kupata kipato cha kuridhisha huku wakiiomba Serikali endapo inawezekana wangewezeshwa kupata mashine nyingine.
"Mwanzoni maisha yetu yalikuwa ya wasiwasi kwa sababu tulipoanzia tulikuwa tunatwanga kwa vinu na soil tunapata unga tunaenda kuosha alafu badae tunachukua dawa tunachenjua tunapata dhahabu lakini kwa maumivu makubwa sana kwasababu tulikuwa tunatumia nguvu",amesema Bwana Mnoga ambae pia ni mjasiriamali na mwanakikundi Tujiendeleze.
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/a/AVvXsEiPxVAGA04iXSrIkhBXA07BV4LgZWJ65jp8TQDAwyUiWXqT3Mm1211PpO0Wu7WdzzMcZxtxuUelWvqBJy2muwb6acIYnYf6vol-GkQ6jXV---HHBrAttX7GV_nrP4QKuBNl9zdwTvfVu4txR4t5V9R7-G3NJo9jqJUI9G9EfpVvJAKbvNggDrE55gSK=w640-h360)
Bwana Joshua Mnoga,mjasiriamali na mwanakikundi Tujiendeleze.
Hata hivyo wamesema kupitia mradi huo wameweza kuajili watu wengine watatu akiwemo opareta,
"kiujumla tumetoa ajira nyingi kwa sababu kama unavyoona watu ni wengi wanafanya kazi zao kujipatia kipato ila sisi ambao tumewaajili na kuwalipa ni hao watatu",amesema Adam Isaac mjasiriamali na mwanakikundi Tujiendeleze.
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/a/AVvXsEj4fuiaMXW4morvpgD4GPd-dol1x2HnqsfDqlZqv8L5Hv_DnlShNZxpEyiExY2XNsz3OBywkhwQg41KolGwbpOues4FeUU2g_XVptvtf_G_A2p-NYDEgnUtl1dvBz7LDamGrHDjK3vhLUmmSRAthzf0e5oieLTRVPQl8GklmhnxE1gJXmJcJeghlay2=w640-h360)
Adam Isaac mjasiriamali na mwanakikundi Tujiendeleze.
Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Mpanda Marieta Mlozi amesema kuwa Kikundi Cha watu wenye Ulemavu cha Tujiendeleze kimekopeshwa na Halmashauri kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza walikopa kiasi Cha Tsh Mil 3 na kiliweza kurejesha kwa wakati.
"Kwa maelezo yao wanasema hizi fedha zimeweza kuwasaidia kuboresha makazi yao na miradi midogo kama ya ufugaji wa Kuku na Mbuzi",amesema Marieta.
Bi.Marieta anaongeza kuwa baada ya kuona kuwa kikundi cha Tujiendeleze wamekidhi vigezo Halmashauri iliweza kuwakopesha tena kiasi cha Tsh Mil 10 katika awamu ya Pili ambazo wamenunua Mashine ya kusagia dhahabu ambapo fedha hizo walipewa mnamo mwezi Septemba 2021.
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/a/AVvXsEh3pAltVkW9EHBvklCYCee_jEJTFDTTowkhDfP6A_RnNMLvnumsXVt3SFM4QtaYFijEawLk5G7jLZV4kDyywcK2nekqwR93ExcaagaP1fgapmVFw7l1q-IcS_IkuuvaCfcci0JkTH1L-WmzPXoyE-IHNP3dne9yf1pVWHb5KpqRuiGouW8s1Ir6vpR9=w640-h360)
Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Mpanda Marieta Mlozi akizungumzia Kikundi cha TUJIENDELEZE.
Katika ziara ya Ukaguzi wa Miradi kwa Kamati ya Fedha na Utawala iliyofanyika leo Januari 21,2022 Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mpanda Haidary Sumry amepongeza hatua ya Kikundi hicho kwa kutumia vizuri Mkopo waliopewa na Serikali na kutoa wito kwa watu wengine wenye ulemavu kujiunga kwenye vikundi mbalimbali na kufanya shughuli za maendeleo zitakazo wawezesha kupata Mkopo wa 10% unaotolewa na kila Halmashauri ili kujinasua kiuchumi.
"wajiunge kwenye vikundi lakini wawe na shughuli kwa sababu hatumpi mtu pesa ambaye hana shughuli,na zikikaguliwa zikionekana ni shughuli zenye tija sisi tuko tayari kuwapa mikopo,na kwenye kipengele hicho cha walemavu kwakweli wanaokuja ni wachache sana..,kwahiyo nafasi bado wanayo"Amesema Mstahiki Meya Sumry.
"Mwezi wa 9 tulitoa Mil 245 za Mikopo kama Manispaa,na tunakaribia mwezi wa pili mwanzoni tutatoa tena pesa,kwahiyo nafasi bado wanayo",aliongeza.
MWISHO.
Comments
Post a Comment