Mkurugenzi wa asasi ya Usevya Development Society (UDESO) Eden Wayimba
Wazazi na walezi Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe Mkoani Katavi wameombwa kushirikiana na vyombo vya sheria katika kufichua matukio ya ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia pindi yanapotokea katika jamii ili kutokomeza vitendo hivyo.
Hayo yamejiri katika hafla ya uzinduzi wa Mradi wa kushiriki kutokomeza na kupinga Ukatili na Unyanyasaji wa Kijinsia,Mimba na Ndoa za Utotoni ulioandaliwa na Taasisi ya Usevya Development Society (UDESO) kwa Ufadhili wa Taasisi ya Women Fund Tanania (WFT) na kufanyika katika Ukumbi wa Kapalale uliopo Halmashauri hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wadau wamesema kuwa wanakutana na changamoto pale wanapobaini vitendo hivyo ambapo wazazi na walezi hushirikiana na mhalifu kuficha uovu uliotokea.
"Levo yangu ni kumpelekea Mtendaji wa Kata ambae ni bosi wangu,lakini kesi ile ukipeleka pale inavurugwa vurugwa tuu bila sababu yoyote sijui kama inaenda Polisi,mimi nitaendelea kumfuatilia mtoto mpaka ntaitwa mnoko,naomba tujifuze watoto wana faida sana badae",amesema Patrick Nzowa Mkuu wa Shule ya Sekondari Usevya.
"Kazi yetu baada ya kuletewa taarifa ni kwenda kumkamata mhalifu,baada ya kumkamata familia au mzazi wanakwenda kuelewana na mhalifu,kesi ikishafika mahakamani mtoto anafundishwa kusema nililazimishwa nimtaje fulani,mwisho wa siku ushahidi unapotea",amesema Daniel Richard Mtendaji Kijiji cha Kibaoni.
Nae Damary Thomas ambae ni Mjumbe wa Bodi ya UDESO amesema kumekuwa na kasumba ya watu kuchukua mabinti wadogo wenye umri wa kusoma na kuwafanyisha kazi za majumbani hivyo kuishauri Serikali kwa kushirikiana na wananchi kufichua wanao watumikisha watoto.
Mila Potofu za pamoja na lugha za "Mchumba mchumba" pia zimetajwa na Jerome Mwakalemba kuwa sehemu ya chanzo cha matukio ya ubakaji na unyanyasaji wa Kijinsia katika Halmashauri hiyo.
Mkurugenzi wa asasi ya Usevya Development Society (UDESO) Eden Wayimba amesema lengo la mradi huo ni kutokomeza tatizo la Mimba za Utotoni na Ukatili wa Kijinsia uliokithiri katika Mkoa wa Katavi hivyo wanaamini kampeni hiyo itapunguza tatizo kwa kiasi kikubwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe Godfrid Nkuba amesema wao kama Serikali kwa kushirikiana na wananchi pamoja na taasisi hiyo wanaamini watakwenda kutokomeza na kupinga Ukatili na Unyanyasaji wa Kijinsia,Mimba na Ndoa za Utotoni katika Halmashauri hiyo kwani wamekuwa wakifanya hivyo katika utoaji wa Elimu hadi kwa Waendesha Pikipiki maarufu Bodaboda ambao pia wanatajwa kuwa sehemu ya chanzo cha Mimba za Utotoni.
Mimba 2965 sawa na 27% zilibainika katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe kwa Mwaka 2019/20 na Mimba 2628 sawa na 23% kwa Mwaka 2020/21.
Comments
Post a Comment