![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhk4IUHMKBL6qHTec3YgnO6GyA779HUqLevQLBkbH0HVY2mm9BwfEqnNFhaHIfqnvoZfQZlRzknI9MkZ391uLypF2vHXNWGj76RLyNxAWoB67cb_5rY5-eQCPDnaGw91IE_AjZ-pxxNErI/w640-h360/vlcsnap-2021-09-28-02h04m38s237.png)
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhqS8oef3EvBDlDGWhzMzCr3pDWKjYQ0w-UUvy52O2OGq4t85ggyYCFlGSEodRPp1pi9J0mEgys_M5YhMbcr67pUpGZrmeqqUosXR49hZ2-XrCEsUVkXi2TUVBzGfaEjmOHOCb7-QU0APw/w640-h360/vlcsnap-2021-09-28-02h04m03s141.png)
Pichani ni Waandishi wa Habari wakifatilia Mkutano wa Maadhimisho ya Miaka 20 ya NHIF katika Ukumbi wa LAPF Jijini Dodoma Septemba 24,2021.
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgnqH8RG1lY0ehRduYsTXAfBNi83aJ8sfMJdXbLP-bOzPZgtcL0yUqSeeOWL-nFYcUi43DvuR7vKI2lAJuBkkUhMontvCAuVX-H3e-fgPFJc3GJfJ3i0dladyBVQ8wsNyRmMjmFN3wPgXw/w640-h360/vlcsnap-2021-09-27-12h24m34s135.png)
Mkurungenzi wa rasilimali na Utawala NHIF Bw.Charles Lengeju akizungumza jambo wakati akifungua Mkutano na Waandishi wa Habari Nchini katika Maadhimisho ya Miaka 20 ya NHIF.
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhwsboDb0KZ88T31dXkDrPs_ikW-f_uZpaslPC9gMguc0mDQ-cx-1r0F2nYwvGhZeIAHjUjx1oYhlM4AbJk8xvAkXRuiKqcOLxqfG_I5bie_ICruWK24KDDYP0BEFn1vB2Iw7HgTZid9Gc/w640-h360/vlcsnap-2021-09-27-11h13m46s150.png)
Mkurungenzi wa Huduma za Uanachama wa NHIF Bw.Christopher Mapunda akifafanua jambo mbele ya Waandishi wa Habari Nchini katika Maadhimisho ya Miaka 20 ya NHIF.
*********************************
Na Aidan Felson,Site Tv-Katavi
Katika kuhakikisha Afya za Watanzania zina imarika,Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umekusudia kupeleka muswada Bungeni ili itungwe Sheria ya Bima ya Afya kwa wote.
Akifungua Mkutano wa Waandishi wa Habari Nchini,katika Mkutano wa kuadhimisha Miaka 20 ya NHIF ya huduma katika Ukumbi wa LAPF Jijini Dodoma,Mkurungenzi wa rasilimali na Utawala NHIF Bw.Charles Lengeju kwa niamba ya Mkurungenzi Mkuu wa NHIF Bernard Konga alisema,lengo kuu la Mfuko ni kutaka kila Mtanzania awe na Bima ili iwe vyepesi kupata Matibabu pindi Ugonjwa unapotokea kwa dharula wakati huna Pesa.
Bw.Lengeju alisema ni matarajio yao kuona Wadau wakiunga Mkono Muswada huo utakapopelekwa Bungeni kutokana na nia thabiti ya Mfuko kunusuru Afya za Watanzania.
Alisema kutokana na changamoto kadhaa,Mfuko umeamua kuboresha huduma kwa Wanachama kwa kupanua wigo wa huduma zitolewazo kwenye kitita cha Mafao cha Mfuko ambapo kwa sasa huduma nyingi zimeongezwa ikiwemo Matibabu ya Moyo,kusafisha Figo na Vipimo vikubwa vinalipiwa.
"Vile vile tumeshirikiana na Mabenki ili kuwezesha Wananchi kujiunga na Mfuko kwa kulipa kwa kudunduliza,sababu wengine ilionekana kwamba mpaka niweke fedha ifike kiwango kile kinachotakiwa kulipwa wengine wanashindwa"-Alisema Lengeju.
Naye Mkurungenzi wa Huduma za Uanachama wa NHIF Bw.Christopher Mapunda alisema toka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) uanzishwe Mwaka 2001 Idadi ya Wanachama wachangiaji kwa Mwaka 2001/02 imeongezeka kutoka 164,708 hadi 1,212,519 Mwaka 2020/21.
Mapunda alisema kwa Mwaka 2001/02 ni Asilimia 2 tu ya Wanufaika wa Bima ya NHIF kwa Watanzania wote waliokuwa Wanaufaika ukilinganisha na Asilimia 8 kwa Mwaka 2018/19-2020/21 huku Vituo vilivyosajiliwa vya kutolea huduma vikitajwa kuongezeka kutoka Vituo 3,197 kwa Mwaka 2001/02 kufikia Vituo 8482 Mwaka 2020/21.
Alisema NHIF ipo katika mikakati ya kufikia lengo la Afya kwa wote ambapo Moja ya mikakati ni pamoja na kuhakikisha wanaongeza vifurushi kwa makundi mbalimbali ya Wananchi kujiunga na Bima ya Afya,kuongeza Vituo vya kutolea huduma za Afya,kuimarisha mifumo ya TEHAMA sanajari na kuimarisha Miundombinu ya utoaji huduma.
"Tunaendelea kuimarisha mifumo ya TEHAMA ya kusajili Wanachama hasa katika kipindi hiki cha tatizo la UVIKO-19,sio lazima sana Mwanachama aje Ofisini,anaweza akafanya maombi huko aliko. Sio lazima Mtoa huduma afike Ofisini aweze kufanya usajili wa Kituo chake,anaweza akafanya usajili huko huko alipo"-Alisema Mkurungenzi wa Huduma za Uanachama wa NHIF Bw.Christopher Mapunda.
Hata hivyo alifafanua kuhusu changamoto mbalimbali zinazolalamikiwa na Wadau ikiwemo kupungua kwa baadhi ya Dawa na Vipimo vilivyokuwa vikitolewa awali kuwa sababu kubwa ni kutokana na mwongozo mpya wa Tiba na orodha ya Taifa ya Dawa Muhimu Nchini wa Mwaka 2018 kuwa na mapungufu ya aina na Idadi ya Dawa na Vipimo jambo ambalo limeshafanyiwa kazi kwa kusitisha matumizi ya mwongozo huo.
Aidha,hoja nyingine iliyofanyiwa kazi ni suala la kuondolewa kwa kundi la Watoto waliotimiza Miaka 18 au zaidi kama wategemezi ikiwa ni utekelezaji wa sharti la Kisheria ya Mfuko kifungu cha 15(3) cha Sheria ya Mfuko,sura 395 kwa kurejesha kundi la Watoto wategemezi walioondolewa ambao hawajatimiza Miaka 21 sambamba na kuwasilisha mapendekezo ya mabadiliko ya Sheria na kanuni ya Mfuko kuongeza Umri wa Watoto wategemezi kutoka Miaka 18 hadi 21.
Kwa upande wao Waandishi wa Habari wamewashauri Viongozi kufanya ufuatiliaji wa malalamiko yanayotolewa na Wateja wao juu ya vitendo vya urasimu kwa baadhi ya Watoa huduma za Afya waowaambia Wateja wa Bima kuwa Dawa fulani hakuna hali ya kuwa ipo badala yake anapewa kipaumbele aliyekuja na Pesa mkononi.
Hata hivyo wameshauri Viongozi wa Mikoani kutembea Vijijini kwa ajili ya kutoa Elimu kwa kuwa wapo baadhi ya Wananchi wenye matatizo na hawajui namna ya kupata Bima hiyo kwani ingewasaidia kupunguza ghalama za Matibabu kutokana na hali ya Uchumi.
Wanahabari hao pia wameshauri ni vizuri Viongozi hao kuwa na tamaduni za kuandaa mikutano ya kutoa Elimu yenye ajenda zihusuzo Bima badala ya kuvizia Mikutano ya kualikwa kama Wadau.
Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) ni Taasisi ya Umma iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria sura 395 na kuanza utekelezaji wake Julai 1,2001 hiyo ikiwa ni matokeo ya maboresho katika Sekta ya Afya yaliyoanza Miaka 90 kwa lengo la kusimamia upatikanaji wa huduma bora za Afya kwa Watumishi wa Umma na Wategemezi wao ambapo baadae yalijumuishwa Makundi mengine ya Wananchi wanaojiunga kwa hiari.
Makundi yanayolengwa na Mfuko ni pamoja na Makampuni Binafsi ambayo yanajiunga kwa utaratibu wa Mwajiri na Mwajiriwa,kundi la Watoto chini ya Umri wa Miaka 18,Wanafunzi kuanzia Elimu ya awali hadi Vyuo vya Elimu ya Juu,Wakulima kupitia Vyama vyao vya Ushirika vilivyosajiliwa katika mpango Ushirika Afya.
Kadhalika Makundi ya Wananchi katika Makundi ya Kijamii na ya kiuchumi kama vile kundi la Wamachinga,Boda boda,Mama Lishe n.k,Familia au Mtu Mmoja kupitia mpango wa Vifurushi ambapo lengo la makundi hayo ni kutaka kila Mwananchi kuwa na fursa ya kujiunga kwa ghalama nafuu na hivyo kuwa na uhakika wa Matibabu kwa kutumia Bima ya Afya wakati wowote.
Akifunga Mkutano huo wa Siku Mbili uliofanyika Septemba 24-25/2021 kwa kuhitimishwa kwa Bonaza Mgeni rasmi katika Mkutano huo Mkurungenzi wa rasilimali na Utawala NHIF Bw.Charles Lengeju alisema kwa kutambua umuhimu wa Waandishi wa Habari wataendelea kushirikiana katika kutoa Elimu ili Jamii ijue faida za kukata Bima mapema badala ya kusubiri Ugonjwa ndipo Mtu anapokumbuka kukata jambo ambalo haliwezekani.
MWISHO.
Comments
Post a Comment