Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa 5 kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya mauaji,kujeruhi na kuingiza bidhaa Nchini bila kulipia ushuru.
Kuhusu taarifa za Mauaji,Jeshi la Polisi Mkoani humo limesema Watuhumiwa Watatu ambao ni Lusajo Mwaijobelo (32),Naboti Sanga (44) na Christina Chaula (50) wote wakazi wa Kisyosyo-Matema Wilaya ya Kyela,wanashikiliwa kwa tuhuma za tukio la mauaji ya Mwanamke aitwaye Elizabeth Mwaike (22) Mkazi wa Kisyosyo.
Watuhumiwa wamekamatwa Mei 28,2021 majira ya saa 18:30 jioni katika Kijiji cha Kisyosyo,Kata ya Matema,Tarafa ya Ntebela,Wilaya ya Kyela,Mkoani Mbeya,ambapo katika Machimbo ya Kokoto ya kampuni ya Kichina,Marehemu alikutwa eneo hilo akiwa ameuawa kwa kupigwa kitu kizito kichwani umbali wa mita 500 kutoka Nyumbani kwake.
Chanzo cha tukio hilo kimeelezwa kuwa ni wivu wa kimapenzi na upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.
Katika tukio lingine,Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya linamshikilia Furaha Shipindi (37) Mkazi wa DDC-Mbalizi kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya kujeruhi.
Mtuhumiwa alikamatwa Mei 28,2021 majira ya saa 21:00 usiku,mtaa wa DDC katika Mji Mdogo wa Mbalizi,Kata ya Utengule,Tarafa ya Usongwe,Mkoa wa Mbeya.
Katika upekuzi,Mtuhumiwa alikutwa na shoka dogo,nondo iliyochongwa mbele na begi dogo lenye nguo anazobadilisha kuvaa kila baada ya tukio.
Aidha,Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Mfanyabiashara aitwae Philip Peter (49) mkazi wa Jijini Mbeya kwa tuhuma za kuingiza bidhaa Nchini bila kulipia ushuru pamoja na kuingiza bidhaa zilizopigwa marufuku.
Mtuhumiwa alikamatwa Mei 28,2021 majira ya saa 05:00 alfajiri Kijiji cha Bujinga, Kata ya Bagamoyo, Wilaya ya Rungwe,Mkoani Mbeya akiwa na Gari yenye namba za usajili T.259 BLA aina ya Toyota Hilux Pickup akiingiza bidhaa mbalimbali Nchini akitokea Nchini Malawi bila kulipia ushuru.
Bidhaa alizokamatwa nazo ni pamoja na Sukari katoni 30,Uyoga mifuko 20,Mafuta ya kula ndoo 10 kila moja lita 20 na Pombe kali zilizopigwa marufuku Nchini aina ya Fighter Vodka katoni 60 na taratibu za kiforodha zinaendelea.
Comments
Post a Comment