Na, Swaum Katambo-Katavi
Mkuu wa Mkoa wa Katavi Juma Homera ametoa siku 7 kwa wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri za Tanganyika,Nsimbo na Mlele kuwasilisha fedha za ujenzi wa Eneo la maonesho ya wakulima Nanenane lililopo Kata ya Kabungu Wilayani Tanganyika.
Maagizo hayo yametolewa leo Aprili 19,2021 katika kikao cha wadau wa Sekta ya Kilimo Mkoa wa Katavi kilichofanyika katika Ukumbi wa Idara ya Maji uliopo Manispaa ya Mpanda mara baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Afisa Kilimo wa Mkoa Faridu Mtiru alipokuwa akiwasilisha maadhimio yatokanayo katika kikao cha wadau wa Kilimo kilichoketi mnamo Desemba 16,2020.
Hata hivyo RC Homera amewaambia Wakuu wa Wilaya pamoja na Wakurugenzi endapo watashindwa kutekeleza agizo hilo waandike maelezo ya kushindwa kutekeleza huku akiwapongeza Manispaa ya Mpanda pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe ambao wamekwisha wasilisha fedha zao.
Kadhalika katika kikao hicho kilichokutanisha wadau wa Sekta ya Kilimo Mkoa wa Katavi, kilipata kuzungumzia baadhi ya changamoto zinazowakabili wakulima zikiwemo ucheleweshwaji wa malipo ya wakulima katika vyama vya msingi pamoja na ununuzi wa mazao kwa bei ndogo ambapo
Mhasibu wa Bodi ya Nafaka na Mazao mchanganyiko Mkoani Katavi Zawadi Mrisho amesema wanatarajia kununua Tani 1000 za mazao ya Alizeti,Karanga,Maharage,Mahindi na Mpunga kwa bei isiyowaumiza wakulima.
Kwa upande wake Mrajis Msaidizi Mkoa wa Katavi Ibrahim Kakozi amesema Mkoa unatarajia kukusanya Tani 6937 za Ufuta kupitia vyama vya Ushirika, jumla ya Vyama vya Ushirika 19 vitashiriki katika zoezi la ukusanyaji na uuzaji wa Ufuta ghafi kwa msimu wa Mwaka 2021/2022.
MWISHO.
Comments
Post a Comment