Na Swaum Katambo-Katavi
TAKUKURU Mkoani Katavi imeokoa na kurejesha fedha kiasi cha Shilingi Mil 10 kwa Mwalimu George Gabriel Kanyukamalunde ambaye ni mstaafu aliyedhulumiwa fedha za mafao yake baada ya kukopa fedha kwa nyakati tofauti kutoka kwa mkopeshaji mmoja Mkoani hapa.
Akitoa taarifa mbele ya waandishi wa Habari Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Katavi Christopher Nakua amesema mnamo Disemba 3, 2020 walipokea taarifa kutoka kwa Bi. Catherine Mlenga ambaye ni mke wa Mwl Kanyukamalunde juu ya madai hayo ambapo baada ya Mkopeshaji huyo kumkopesha mzee huyo alichukua Kadi yake ya Benki pamoja na namba za siri ambayo ndiyo iliyotumika kuchukulia fedha mara baada ya kiinua mgongo kutoka.
Ameongeza kuwa baada ya uchunguzi kukamilika mtuhumiwa alikiri makosa na kuahidi kumrejeshea mlalamikaji kiasi cha Shilingi Mil 20 ambapo ni tofauti ya fedha ambazo ilikuwa ni kama dhuluma kwa mlalamikaji kwani kiasi hicho cha fedha hakikuwa na maelezo ya kutosha kama ni riba au ni nini ambacho kilirejeshwa Februari 23, 2021.
“Mtuhumiwa alirejesha kiasi cha shilingi Mil 10 taslimu na kiasi kilichobaki cha shilingi Mil 10 atarejesha Aprili 30, 2021 ili kukamilisha kiasi cha shilingi Mil 20 alichomdhulumu Mwl Kanyukamalunde” Amekaririwa
Kwa upande wa wanafamilia ya Mwl Kanyukamalunde ambao ni Bi. Catherine Mlenga na mtoto wake Genuine Kanyukamalunde wameishukuru TAKUKURU kwa kusaidia kupatiwa msaada huku wakisema pesa hizo zitakwenda kusaidia matibabu ya mzee wao kwani baada ya kudhulumiwa pesa zake alipata mshtuko na kumsababishia maradhi.
Katika hatua nyingie TAKUKURU Mkoa wa Katavi imemkamata Egid Damas Ntila ambaye ni Kaimu Katibu wa Serikali ya kitongoji cha Magula kilichopo Katika kijiji cha Mtisi, Kata ya Sitalike Wilayani Mpanda kwa kuomba Rushwa ya shilingi 300,000 na kupokea Rushwa ya shilingi 50,000 katika eneo la Soko Jipya la kitongoji cha Magula.
TAKUKURU Mkoa wa Katavi inatoa wito kwa wananchi kama kuna ulazima wa kukopa ni vizuri kwenda kukopa kwenye Taasisi za kifedha zilizo rasmi na zinazofuata sheria, taratibu na miongozo ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT)
MWISHO
Comments
Post a Comment