Na Swaum Katambo,
Mpanda-Katavi
Jumla ya Wahitimu 40 wa Mafunzo ya Huduma ya kwanza yaliyotolewa na Chama cha Msalaba Mwekundu (Red Cross) Manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi wametunukiwa Vyeti baada kushiriki Mafunzo ya takribani Siku 10 yaliyoanza Oktoba 5 na kumalizika Oktoba 16 katika Ukumbi wa Serena uliopo Kata ya Makanyagio. Akihitimisha Mafunzo hayo katika hafla iliyofanyika kwa Wahitimu wa Mafunzo hayo Mgeni rasmi ambaye pia ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Katavi Dkt. Omary Sukari,amepongeza hatua ya Red Cross Tanzania kuona umuhimu wa kutoa mafunzo hayo kwa Wanakatavi kwani kabla ya mafunzo hayo Mkoa mzima ulikuwa na Watu Watatu tu waliopata mafunzo hayo kiusahihi huku akiahidi kuwa Sekta ya Afya ipo tayari kutoa vifaa maalum vya huduma ya kwanza kwa shirika la red Cross Mkoani Katavi kutokana na uwepo wa uhaba wa Vifaa. Dkt. Sukari pia ameahidi kuandika barua zitakazozifikia Taasisi zote zilizopo Mkoani humo ili kuhakikisha Elimu ya Huduma ya kwanza (Red Cross) inatolewa kwa Watumishi pamoja na Watu wengine walio tayari kupata Elimu hiyo wakiwemo Wahudumu wote wa Afya ili kuendelea kuokoa Wanachi wa Mkoa wa Katavi. Awali akitoa taarifa kwa mgeni Rasmi Mwenyekiti wa chama hicho Mkoani Katavi Shebby Mloti amesema Mafunzo hayo yamehusisha Wananchi wa kawaida,na ameongeza kuwa kukamilika kwa mafunzo hayo kutasaidia kuunda kikosi kazi cha Mkoa katika kutoa huduma ya kwanza kwa Jamii hasa sehemu zenye mikusanyiko ya Watu wengi na kumuomba Mgeni rasmi kupitia Ofisi ya Mganga Mkuu itoe matumaini kwa wahitimu hao. Baadhi ya Wahitimu wa Mafunzo hayo wamelishukuru Shirika la Red Cross Tanzania kwa kuwapa mafunzo yaliyowapatia uzoefu wa kutoa Huduma ya kwanza huku wakiiomba Taasisi hiyo kuendelea kutoa Mafunzo kwa Taasisi zingine. Chini ni Picha mbalimbali zikionesha Matukio ya uhitishwaji wa mafunzo ya Huduma ya kwanza yaliyotolewana Shirika la Msalaba Mwekundu (Red Cross Tanzania)yaliyofanyika katika Ukumbi wa Serena Manispaa ya Mpanda
|
Comments
Post a Comment