Aliyesimama ni msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Songea mjini akifungua mafunzo ya siku tatu kwa wasimamizi wasaidizi ngazi ya Kata Manispaa ya Songea
MSIMAMIZI wa Uchaguzi Jimbo la Songea mjini mkoani Ruvuma Tina Sekambo amewatahadharisha wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Kata katika Manispaa hiyo kuepuka migogoro na vyama vya siasa kwa kwa kusimamia mchakato wa uchaguzi kwa mujibu wa sheria za Tume ya Uchaguzi.
Sekambo ametoa tahadhari hiyo kwenye ukumbi wa Manispaa hiyo mjini Songea, wakati anazungumza kabla ya kufungua mafunzo ya siku tatu kwa wasimamizi wasaidizi kutoka kata zote 21 kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu.
“Tume ya Uchaguzi inasisitiza sana,tusitafute migogoro na vyama vya siasa,tuepuke kabisa migogoro ,uchaguzi asilimia 100 unaendeshwa na sheria ,ukikosea hata nukta ni tatizo,tunatakiwa tusome maelekezo yote vizuri ili kufanya mchakato wa uchaguzi mwaka huu kwa ufanisi’’,alisisitiza Sekambo.
Msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Songea mjini Tina Sekambo akifungua mafunzo ya siku tatu kwa wasimamizi wasaidizi ngazi ya Kata katika jimbo hilo kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea
Msimamizi huyo wa Uchaguzi Jimbo la Songea mjini pia amewataka wasimamizi hao wasaidizi siku ya wagombea kuchukua fomu hadi siku ya uteuzi wanatakiwa kuwepo ofisini muda wote na kwamba siku tatu kabla, wanasiasa wanaruhusiwa kuleta fomu zao na kukaguliwa kubaini iwapo zina makosa au zipo sahihi.
Amesema Tume ya uchaguzi imeamua kutoa mafunzo hayo ya siku tatu ili kufanikisha zoezi la Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ambapo amewaasa kuhakikisha wanazingatia mafunzo yote ambayo watapewa na Tume ya Uchaguzi badala ya kufanyakazi kwa mazoea.
“Hakikisheni mnazingatia matakwa ya Katiba,Sheria,Kanuni zinazosimamia Uchaguzi,maadili ya uchaguzi na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na NEC’’,alisisitiza Sekambo.
Kwa upande wake Afisa Uchaguzi Manispaa ya Songea Christopher Ngonyani amesema mafunzo hayo yameshirikisha wasimamizi wasaidizi 42 kutoka Kata 21 zilizopo katika Manispaa hiyo na kwamba wote walioteuliwa na NEC wamehudhuria mafunzo hayo.
Afisa Uchaguzi huyo amewaasa washiriki wa mafunzo kuzingatia mafunzo wanayopewa na kuhakikisha kila msimamizi anayatambua maeneo ambayo atafanyia kazi ikiwemo miundombinu ya kufika katika kata na vituo vya kupigia kura.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya wasimamzi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata Manispaa ya Songea wakipata mafunzo kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea yanayotolewa na Tume ya Uchaguzi (1)
Wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata katika Manispaa ya Songea wameapishwa na Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi mkoani Ruvuma Livini Lyakinana.
Uchaguzi Mkuu wa Rais,wabunge na madiwani unatarajia kufanyika nchini Oktoba 28 mwaka huu.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari wa Mkoa wa Ruvuma
Comments
Post a Comment