Na Mwandishi Wetu,
Katavi.
Wakulima Mkoa wa Katavi wameombwa kuachana na kilimo cha
mazoea ambacho hakimkomboi mkulima
kiuchumi na badala yake kumfanya kuzalisha mazao ya chakula na biashara
yasiyokuwa na tija huku yakimwacha masikini.
Kauli hiyo imetolewa jana kwenye ukumbi wa Idara ya Maji
Manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi na Afsa Masoko na Mauzo wa ETC Agro Tractor,Zahra
Salum wakati akizungumza na wadau wa kilimo mkoani humo ambapo aliwaambia kuwa
kilimo pekee chenye tija kitamkomboa mkulima kutoka kwenye umasikini.
Zahra aliweka wazi kuwa kwa kutambua juhudi zinazofanywa na
serikali ya awamu ya tano chini ya rais Dkt John Magufuli ya kuadaa sera
madhubuti za kuhakikisha sekta ya kilimo inakua kwa kasi na kumfanya mkulima
kupiga hatua za maendeleo ya kiuchumi ndio zimeifanya Kampuni ya ETC Agro
Tractor kwa kushirikiana na Benki ya CRDB Tawi la Mpanda kuandaa mfumo ambao
utamfanya mkulima kupata zana za kilimo za kisasa,
Mfumo huo ambao umewekwa na ETC Agro Tractor ni kumpatia
mkulima matrekta kwa bei nafuu sambamba na kuigia ubia na Benki ya CRDB ambapo
mkulima ataweza kukopeswa bila masharti ili wakulima wadowadogo waweze kunufaika.
“…mikopo hii ya matrekta kulingana na mkataba tuliofanya na
CRDBank mkulima hatakiwi kutoa dhamana ya aina yoyote bali dhamana yake itakuwa
ni trekta hilohilo ambalo anapokabidhiwa,Kadi ya trekta itabaki benki kwa muda
wa miaka mitatu hadi pale mkulima atakapomaliza kulipa deni ndipo atakabidhiwa
na kumiliki mojakwa moja”Alisisitiza Afsa masoko huyo.
Vilevile Zahra alisema kuwa mikopo ya matrekta inakuwa nafuu
kwa sababu wakulima watapaswa kufanya marejesho ya malipo ya fedha mara moja
kwa kila mwaka,kulipia kiasi cha fedha asilimia 35 ya thamani ya trekta pamoja
na mkulima kuwa na hekali 20 za kwake binafsi au za kukodi kwa mkataba kwani
ndizo zitambulisha mwananchi kama ni mkulima na kuepuka watu walanguzi.
Meneja wa Benki ya CRDB Tawi la Mpanda Hamand Masoud alisema
kuwa mkoa wa Katavi kwa sasa unapaswa kupiga hatua kubwa kwenye sekta ya kilimo
ili mkulima aweze kunufaika kwa kuzalisha mazao yenye tija.
Masoud alisema hatua ambazo mkoa unapaswa kuchukua ni pamoja
na wakulima kuachana na zana duni za kilimo kama vile majembe ya mkono au
yakukokotwa na n’gombe.
Aidha Meneja huyo alifafanua kuwa Mkoa wa Katavi umebarikiwa
kuwa na mvua za kutosha na ardhi yenye rutuba,Hivyo wakulima wanapaswa
kuchangamkia fursa hizo za kutumia zana za kilimo za kisasa ili mkoa uweze
kuongoza kitaifa kwenye uzalishaji wa mazao ya chakula ikiwa na mkulima kukuza
uchumi wake binafsi na taifa kwa ujumla.
Gabriel Simon Mkazi wa Kijiji cha Mwese Wilaya ya Tanganyika
Mkoa humo akizungumza kwa niamba ua wakulima alipongeza Taasisi za Kibeki
pamoja na makampuni yanayosaidia wakulima kujikwamua kiuchumi.
Comments
Post a Comment