Na John Alex Mganga
Nsimbo -Katumba.
Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Mh.Bi Jamila Kimaro amewataka Wadau wa Elimu Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo kuyafanyia kazi kwa vitendo maazimio mbalimbali yaliyotolewa katika kikao hicho ili kuinua ubora wa Elimu Nsimbo.
Mh.Kimaro ametoa rai hiyo wakati akifunga kikao cha wadau wa Elimu Nsimbo Kilichofanyika Agosti 18 ,2020 katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari Katumba kwa lengo la kujadili changamoto mbalimbali na kuzipatia ufumbuzi ili kuinua Ubora wa Elimu ndani ya Halmashauri ya Nsimbo
Kudumisha Ushirikiano baina ya Walimu na Wazazi katika kuhakikisha kuwa changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya Elimu ikiwemo utoaji wa chakula inapatiwa ufumbuzi,Uzingatiaji utoaji wa Elimu ya Awali,Uboreshaji wa miundombinu pamoja na kuzingatia utekelezaji wa maazimio yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Katavi Cde.Juma Zuberi Homera ni maazimio yaliyoazimiwa na Wadau wa Elimu Nsimbo katika kikao hicho.
Akizungumza ukumbini hapo Mh.Kimaro mesema ni muhimu kwa Wadau walioshiriki katika Kikao hicho Nsimbo kuyachukua maazimio yatokanayo na kikao hicho na kuyapeleka mpaka ngazi ya Kijiji ili kuwapa fursa Wananchi kushiriki katika kutekeleza kwa Vitendo yale yaliyoazimiwa jambo litakalosaidia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto mbalimbali zinazoikumba Sekta ya Elimu Nsimbo.
Mh.Jamila ametoa wito kwa Wadau wa Elimu kuhakikisha kuwa wanakomesha tabia ya kuwatumikisha Wanafunzi katika shughuli binafsi za walimu ama za Wananchi na badala yake kuhakikisha kuwa Wanafunzi hao wanashiriki katika shughuli za Shule zikiwemo zile za Kilimo katika maeneo ya Shule yaliyotengwa ili kujihakikishia uwepo wa Chakula Mashuleni.
Amewataka Wazazi wa Wanafunzi Nsimbo kujitoa kwa moyo kuchangia Chakula Shuleni ili kuwawezesha watoto kupata chakula cha kutosha jambo litalaowawezesha watoto hao kuwa na Afya nzuri hali itakayowaezesha kufanya vizuri katika masomo yao na hivyo kuinua ubora wa Elimu Nsimbo.
Mh.Kimaro amepiga marufuku Wananchi Nsimbo kuwapangisha Wanafunzi hususani wa kike na badala yake washiriki kikamilifu katika kuchangia ujenzi wa Mabweni ya Wanafunzi hao ili kudhibiti vitendo mbalimbali vinavyoathiri masomo ikiwemo mimba kwa watoto wa kike sambamba na kuwaepusha watoto wa kiume kujihusisha na utumiaji wa madawa ya kulenya.
Mkuu huyo wa Wilaya pia amewataka Wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Walimu ikiwa ni sambamba na kujenga mazingira mazuri yatayowezesha Walimu na Watumishi katika Sekta ya Elimu kupenda mazingira ya kazi jambo litakalosaidia kuinua ubora wa Elimu Nsimbo.
Pamoja na mambo mengine Mh.Jamila ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo kwa jitihada mbalimbali zinazofanywa katika kuinua ubora wa Elimu ambapo amewataka Watendaji wa Halmashauri kuongeza juhudi zaidi ili kuhakikisha kuwa wanainua ubora wa Elimu Nsimbo.
Awali akizungumza kwa niaba ya mkuu wa Mkoa wa Katavi katika ufunguzi wa kikao cha wadau wa elimu Nsimbo Katibu Tawala Msaidizi Elimu Bi.Newaho Mkisi pamoja na pongezi amewataka Wadau wa Elmu kuhakikisha kuwa wanatekeleza kwa vitendo maazimio mbalmbali yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Katavi kuinua ubora wa Elimu pamoja na yale yatakayoazimiwa ili kuinua ubora wa Elimu Nsimbo.
Wiki ya Wadau wa Elimu imeanza rasmi Agosti 17 ambapo Kilele chake kinatarajiwa kuadhimishwa Wilayani Tanganyika mapema Agosti 21 mwaka huu ambapo Washindi mbalimbali waliofanya vizuri katika kuinua ubora wa Elimu ikiwemo Ufaulu zitatolewa siku hiyo.
Comments
Post a Comment