Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ameagiza hadi kufikia Julai 25 Mwaka huu Shirika la Bandari,Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),Idara ya Uhamiaji,Jeshi la Polisi,Wizara ya Madini na Tasac wahakikishe wanajenga Mabanda eneo la Karema Wilayani Tanganyika Mkoani Katavi inapojengwa Bandari.
Maagizo hayo ameyatoa Julai 4,2020 wakati akihutubia Wananchi wa Kata ya Karema baada ya kuzindua kwa kuweka jiwe la msingi Ujenzi wa Bandari ya Karema ambayo inajengwa na Serikali kwa kiasi cha zaidi ya Tsh. Bilioni 47.
Waziri Mkuu amesema,Mabanda hayo ni kwa lengo la kujiweka tayari kwaajili ya kupokea wageni kutoka Nchi jirani ya Congo ambayo ndiyo Nchi washirika wakubwa wa Bandari hiyo,ili watakapo wasili eneo hilo taratibu zote zifuatwe zikiwemo za kikodi na kiusalama.
"Hamtaweza kuanza kwa maagizo haya kujenga jengo la matofali,lakini jenga Mabanda yale,ya wakandarasi yale pale,myapange vizuri ili wageni wetu wooote kutoka Congo wakifika,anafika kwanza Uhamiaji,akishamaliza Uhamiaji anaenda TRA,akienda TRA anakwenda kwenye chumba cha Madini kama ameleta Madini tuhakiki na vyumba vyote aingie Nchini Tanzania akiwa na Vibali afanye Biashara zake ili atuletee anacho tuletea"-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika uzinduzi wa ujenzi wa Bandari ya Karema Wilayani Tanganyika Mkoani Katavi.
Aidha,Waziri Mkuu ameziagiza Taasisi hizo zihakikishe zinaweka Maafisa ili kuhakikisha huduma zinatolewa kwa muda mfupi,na amewataka Vijana kuwekeza kwa kujenga Nyumba za kulala Wageni,Hoteli na Saluni za kunyolea Nywele na amewashauri kwenda kwenye Taasisi za kifedha kukopa ili kuwekeza eneo hilo kunakojengwa Bandari kwa kuwa fursa zinakwenda kufunguka.
Waziri Majaliwa amemuagiza Mkandarasi anayejenga Bandari hiyo kujenga usiku na mchna ili ujenzi ukamilike kabla ya Miaka miwili kama alivyo dai.
"Tumeamua kujenga Bandari hii ya hapa Karema, Bandari ambayo itakidhi kupaki Meli zaidi ya Moja,Ndugu Wananchi,Serikali yenu imeanza kutekeleza,nimeenda kukagua,nimeona,na nimeagiza,Bandari hii si yakujenga Asubuhi mpaka Saa kumi na Mbili jioni,Ujenzi uwe usiku na mchana,tunataka tumalize hata kabla ya Miaka miwili hiyo,tunataka tuikimbize Bandari hii,na nimemwambia Mkandarasi na timu yake,wahakikishe wanapeleka taa pale za kujenga usiku na mchana,Hapa Kazi Tu"-Kassim Majaliwa,Waziri Mkuu wa Tanzania.
Hata hivyo,amewasihi Wananchi waliotoa maeneo yao kupisha ujenzi wa Bandari waache kuzuia kwa kuwa hawajalipwa fidia zao kwani Serikali inakwenda kuwalipa na hakuna Mtu yoyote ambaye hatalipwa,na amewasihi Viongozi wa eneo hilo kuwaelimisha ili waruhusu kazi iendelee.
"Wana Karema tumewatengea Bilioni 47,kujenga Bandari hii,wakati naingia nimekuta Bango tulipe Kilomita sijui eneo,Mimi nasema maeneo tuliyoyachukua yote yatalipwa hakuna ambaye atakosa haki yake,tena kisheria,hao wa kulipwa kwa Square meter sio Sheria ya Nchi hii,muhimu ni kufanya tathmini na kulipwa na Fedha tunayo"-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
"Nimesikia mmezuia hapa makatapila yasifanye kazi,msifanye hivyo,msifanye hivyo,narudia kwa mara ya Tatu, msifanye hivyo. Tunajenga Bandari kwa manufaa yenu, tunajenga Bandari kwa manufaa ya Taifa, tunajenga Bandari tuingize Meli kutoka kwa Majirani,tuwakaribishe Wageni kutoka jirani,tupate Fedha tuendelee kujenga Zahanati,tujenge Mashule, tujenge Barabara,hata hiyo Reli itakayojengwa hapa ni kwa Fedha itakayopatikana kwa kujenga Meli hizi,Msizuie kujenga hapa, Fedha yenu MTALIPWA,hii ni Serikali ya ukweli,tumefanya miradi mingapi tutashindwa kulipa Milioni 50!?"-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwaondoa hofu Wananchi waliozuia Ujenzi wa Bandari wakishinikiza malipo yao.
Waziri Mkuu yupo katika ziara ya siku moja Mkoani Katavi ambapo mapema alizindua jengo la Mpanda Plaza liliojengwa kwa ghalama ya Tsh. Bilioni 2.8 ambalo ni kitega uchumi cha Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) kabla ya kuelekea Karema kuweka jiwe la msingi ujenzi wa Bandari ambayo inatarajia kufungua milango ya fursa mbalimbali za uwekezaji.
Pia,Waziri Mkuu amezindua ununuzi wa zao la Pamba kwa Msimu wa Mwaka 2020/2021 kwenye Chama cha Msingi cha Ushirika cha Kasekese Wilayani Tanganyika Mkoani Katavi.
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEg7lDQK_YT6JSWRRdBSSvEb7wpwPp4CCtlyuooL1wGsVjqOQDtsB-6236xuioJBxPmqYTu34a_bJf3toxuGjr5BIsM8li_0kzT_q72wNrRu55vo-ABxKHTrWdlObuT0jQFMhsIyx3fLL4Q/s640/MAJALIWA+22.png)
Kamwelwe alisema katika kupanua fursa za kiuwekezaji Mkoani Katavi,Serikali imekusudia kuupa hadhi ya Kimataifa Uwanja wa Ndege wa Katavi ifikapo Mwezi August Mwaka huu.
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEiZoM0rjdZ5HHXfYixZ96AQUc4jbmJjZeaV03DcsLFmvZI8WoXv89oQKWTACZCSmthQjdusMfA9WvGKPhoJ4xMc-z-SqJ8qhWvh_L-wM1hHA9VtHcJj-U1a8OKrQcH9hXOBk3nKvePmMJ4/s640/drealiner+ed.jpg)
Naye Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mh. Juma Zuberi Homera amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuruhusu fedha zilizotakiwa kuingia katika mfuko wa Serikali baada ya kuuza Magogo yaliyotaifishwa,ambapo alisema pesa hizo zimeelekezwa katika ujenzi wa Hospitali kubwa eneo la Ikola ambayo ujenzi wake utaanza Wiki Mbili zijazo na pesa hizo pia zitatumika kujenga Shule ya Sekondari eneo la Isengule.
"Mh. Waziri Mkuu hivi karibuni tumeuza Magogo,Magogo hayo yalitaifishwa na fedha zilitakiwa ziende katika mfuko wa serikali,kwa dhamira njema ya Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli na kwa usimamizi wako Mh Waziri Mkuu,mkaona kiwango fulani cha pesa kije kijenge Hospitali kubwa katika eneo la Ikola karibu na Isengule"-Mkuu wa Mkoa wa Katavi Juma Zuberi Homera Julai 4,2020.
"Na Mimi nikuhakikishie Mh Waziri Mkuu,Hospitali hii itaanza kujengwa Wiki Mbili zijazo,tunaleta kwanza Milioni Mia Nne,baada ya hapo tutajenga pia na kituo kingine cha Afya katika eneo lile la Kasekese ambalo umeliacha muda fulani uliopita. Lakini pia katika fedha hizo tutaanza ujenzi wa Shule ya Sekondari pale Isengule,ili tuweze kupata Elimu bora na kutoa usumbufu wa kutoka Isengule kuja hapa Karema,hivyo Mh Wazri Mkuu, fedha zile Mh Rais angeamua kuzipeleka sehemu nyingine za uuzaji wa Magogo ambayo yaliyovunwa bila kufuata utaratibu lakini tunapata zaidi ya Milioni 625 na tutazileta zote kwa Wananchi bila chenji"-alisema RC Homera.
Comments
Post a Comment