Na Mwandishi Wetu,Site Tv
Dodoma,Tanzania
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Taifa, wamempitisha Ndugu John Pombe Magufuli kuwa mgombea Urais 2020-2025 wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM kwa kura 1,822.
Mkutano huo umefanyika Julai 11,2020 kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma na kuhudhiriwa na wajumbe wa kamati kuu pamoja na wageni mbalimbali waalikwa kutoka nje na ndani ya Nchi.
Akitangaza matokeo ya kura hizo Mmoja wa wasimamizi wa uchaguzi Ndg. Job Ndugai amesema idadi ya wajumbe waliohudhuri ni 1,822 na hakuna kura iliyoharibika hivyo ameshinda kwa asilimia 100.
Hivyo,rasmi CCM imekamilisha mchakato wa kupata wagombea kwa ngazi ya Urais ambapo kwa Zanzibar atasimama Hussein Mwinyi na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atasimama Rais Magufuli anayeingia katika awamu yake ya pili.
Aidha, Dkt. John Pombe Magufuli amemchagua Mama Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama hicho.
Magufuli amesema katika kipindi cha miaka mitano alichofanya kazi na Mama Samia kama makamu wa Rais amejifunza mengi na ameamua kuendelea naye katika awamu ya pili.
"Nilipomteua Mama Samia kuwa Makamu wa Rais mwaka 2015 sikuujua utendaji kazi wake vizuri lakini ni mchapakazi,anajituma pia ni mzuri,Wasukuma tunapenda weupe,ukiwa na Msaidizi mweupe hata ukiwa na stress zinaisha,nimeamua awe tena Mgombea mwenza"-Dkt. JPM kwenye Mkutano Mkuu Dodoma leo Julai 11,2020.
''Kwa kipindi nilichofanya kazi na Mama Samia nimejifunza mambo mengi sana na kupitia yeye nawahikikishia nitakuwa mtetezi mzuri wa wanawake. Nimekuwa nikimtuma popote hakatai kama na nyie kina Mama mkitumwa hamkatai"-Amesema JPM
Comments
Post a Comment