Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia JUSTINE SADIQ [18] Fundi rangi na mkazi wa Ndola katika Mji Mdogo Mbalizi akiwa na mali mbalimbali za wizi mnamo tarehe 20/07/2020 majira ya saa 15:30 Alasiri katika Kijiji na Kitongoji cha Mwampalala, Kata ya Iwindi, Tarafa ya Usongwe, Wilaya ya Mbeya Vijijini.
Akitoa taarifa hizo Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi wa Polisi SEBASTIAN MBUTA alisema walimkamata mtuhumiwa huyo akiwa mali za wizi ambazo TV moja aina ya “Sansan” nyeusi,Deki moja aina ya “Singsung”,Remote control mbili,na Tarakishi Mpakato aina ya Compac moja pamoja na “adapter” yake zikiwa kwenye mfuko wa sandarusi ambapo thamani ya mali hizo bado haijajulikana na ufuatiliaji unaendelea.
Jeshi la Polisi pia linamshikilia ZUENA SELEMAN [48] Mfanyabiashara, na Mkazi wa Uyole akiwa na vipodozi vilivyopigwa marufuku nchini vyenye viambata sumu.
"Mtuhumiwa alikamatwa mnamo tarehe 21.07.2020 majira ya saa 14:00 Mchana huko maeneo ya Uyole, Kata ya Nsalaga, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya na katika upekuzi uliofanyika dukani kwake alikutwa akiwa na vipodozi vyenye viambata sumu vilivyopigwa marufuku nchini ambavyo ameviingiza nchini kutoka nchini Malawi ambavyo ni Carotone kubwa 06,Carotone ndogo 06,Citrolight 18,Bioclaire 08,Extra Clair 03,Coloderm 07,Maxlight 09,Miki clair kubwa 10,Miki clair ndogo 7,Dawmy 9,Raphid clair 3,G&G 9,Caro light kubwa 01,Calolight ndogo 05,Extra clair ya limao 06,Clairmen 03,Pure white gold 01,Lemon vate cream 10,Carotone b.s.c 12 pamoja na Montclaire 05"alisema ACP Mbuta
Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi wa shauri kukamilika.
Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia MAULID NGOLE [37] Mkazi wa Uyole na FREDI MTEGA [36] Mkazi wa Uyole wakiwa na unga wenye uzito wa Gramu 10 unaodhaniwa kuwa dawa za kulevya aina ya Heroine.
"Watuhumiwa walikamatwa mnamo tarehe 21.07.2020 majira ya saa 14:00 Mchana katika msako uliofanyika huko eneo la Uyole, Kata ya Nsalaga, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya na katika upekuzi walikutwa na unga udhaniwao kuwa dawa za kulevya kete mbili za Heroine"alisema ACP Mbuta.
Vilevile Jeshi la Polisi linawashikilia watuhumiwa wawili IMAN ABDALLAH [21] Mfanyabiashara na mkazi wa Uyole na SNELI ESAU [18] Fundi simu na Mkazi wa Uyole kwa tuhuma za kupatikana na mali za wizi.
"Watuhumiwa walikamatwa mnamo tarehe 21.07.2020 majira ya saa 13:00 Mchana huko eneo la Uyole, Kata ya Nsalaga, Tarafa ya Iyunga, Jiji la Mbeya wakiwa na Tarakishi Mpakato moja aina ya Accer, simu ndogo tatu aina Tecno na simu saba [07] Smartphone za aina mbalimbali ambazo ni mali za wizi".ACP Mbuta.
Kadhalika Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa watatu GIFT MWAKATAGE [22],LAWI MAHALI [25] na JOHN MWALWIBA [34] wote wakazi wa Uyole Jijini Mbeya kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya uhalifu kwa njia ya mtandao.
"Watuhumiwa walikamatwa mnamo tarehe 20.07.2020 majira ya saa 19:00 Usiku katika msako uliofanyika huko eneo la Uyole, Kata ya Uyole, Tarafa ya Iyunga Jijini Mbeya na katika upekuzi walikutwa wakiwa na laini za simu 23 za mitandao tofauti ambazo zimesajiliwa kwa majina ya watu wengine na wamekuwa wakizitumia kufanyia uhalifu wa makosa ya kimtandao kama vile utapeli na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu".ACP Mbuta.
Kaimu Kamanda Mbuta alisema upelelezi wa shauri hilo unaendelea na mara baada ya kukamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na misako dhidi ya mtandao mzima wa wahalifu wa makosa ya kimtandao.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi wa Polisi SEBASTIAN MBUTA anatoa wito kwa jamii kuacha matumizi ya dawa za kulevya kwani ni hatari kwa afya zao.
Aidha Kamanda MBUTA anatoa wito kwa wafanyabiashara kuacha mara moja kujihusisha na biashara haramu ya vipodozi vyenye viambata vya sumu kwani ni hatari kwa afya ya watumiaji.Sambamba na hilo Kamanda MBUTA anatoa rai kwa wananchi walioibiwa mali zao kufika kituo kikuu cha Polisi [Central] na Kituo cha Polisi Mbalizi kwa ajili ya utambuzi wa vitu vilivyokamatwa.
Pia anatoa wito kwa wananchi kuwa makini pindi wanapofanya usajili wa laini zao za simu kuepuka kadi zao kutumika kusajili laini za watu wengine. Pia Jeshi la Polisi linasisitiza wananchi kuendelea kuhakiki usajili wa laini zao kwa kubonyeza *106#, kisha chagua namba 2, ingiza namba ya kitambulisho chako cha NIDA kisha utapata ujumbe utakaoonyesha orodha ya namba za simu zilizosajiliwa kwa kitambulisho chako.
Mwisho anawataka vijana kujenga utamaduni wa kufanya kazi ili kujipatia kipato halali badala ya kujiingiza kwenye vitendo vya kihalifu ambavyo vitawasababisha kupata adhabu kali kwa mujibu wa sheria.
Comments
Post a Comment