Skip to main content

TCRA NA UCSAF WAPEWA MWEZI MMOJA KUJA NA MAPENDEKEZO KUTATUA CHANGAMOTO ZA MWINGILIANO WA MAWASILIANO MIPAKANI.


Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew akiangalia upatikanaji wa huduma ya mawasiliano ya simu katika eneo la Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA) katika lango la Machame lililopo wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro katika ziara yake ya siku mbili katika mkoa huo. Kushoto ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Hai Upendo Wella.



Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew akisisitiza jambo kwa Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi wa KINAPA Angela Nyaki wakati wa ziara yake ya kukagua upatikanaji wa huduma ya mawasiliano ya simu katika eneo la Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro lango la Machame lililopo wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro.


Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew akizungumza na wananchi kupitia redio Boma FM 89.3 inayomilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro wakati wa ziara yake ya kukagua ubora na upatikanaji wa huduma ya mawasiliano ya simu katika Wilaya hiyo.


Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (mwenye suti ya kijivu) akisalimiana na baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mtakuja kilichopo Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro wakati wa ziara yake ya kukagua ubora na upatikanaji wa huduma ya mawasiliano ya simu Kijiji hicho.



Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (kulia) akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Kilimjanjaro Mhe. Stephen Kigaigai ofisini kwake Mkoani Kilimanjaro kabla ya kuanza ziara yake ya kukagua ubora na upatikanaji wa huduma ya mawasiliano ya simu.

Na Mwandishi wetu, HAI

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Mathew ametoa mwezi mmoja kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kutoa maelezo ya kinachosababisha mwingiliano wa mawasiliano katika maeneo ya mipakani na namna bora ya kutatua changamoto hiyo.

Mhandisi Kundo amezungumza hayo katika ziara yake ya kukagua ubora wa huduma ya mawasiliano katika maeneo ya mipakani alipotembelea Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA) kwa upande wa lango la Machame la kupandia mlima huo lililopo Wilayani Hai.

“TCRA na UCSAF nawapa mwezi mmoja mje na majibu ya kutatua changamoto za mwingiliano wa mawasiliano katika maeneo ya mipakani ikiwa ni pamoja na maeneo ya hifadhi za Taifa kwa kuwa kuna maeneo ya mipakani kama Namanga minara ipo lakini bado kuna tatizo la mwingiliano wa mawasiliano”, alizungumza Mhandisi Kundo

Aliongeza kuwa ni muhimu kujiridhisha kama sababu ni nchi ya Tanzania kutii sheria, kanuni na miongozo ya Shirika la Kimataifa linalosimamia Mawasiliano (ITU) kuhusu uwekaji wa miundombinu ya mawasiliano katika maeneo ya mipakani na hatua zilizochukuliwa za kutatua changamoto hiyo ili nchi jirani nazo zifuate utaratibu uliowekwa na ITU.

Alisema kuwa eneo la hifadhi ni eneo nyeti sana kwasababu ni maliasili ambayo nchi inajivunia kama kivutio cha Taifa, chanzo cha ukusanyaji wa mapato kutokana na shughuli za utalii na pia ni urithi wa vizazi vijavyo hivyo ni eneo muhimu kuwa na mawasiliano ya uhakika.

Aidha, katika hatua nyingine Mhandisi Kundo ameutaka uongozi wa hifadhi hiyo kuharakisha mchakato wa utoaji wa vibali vya ujenzi wa minara ya mawasiliano katika maeneo ya hifadhi kwa sababu ni moja ya maeneo ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na watoa huduma kwa kuchelewesha au kukwamisha ujenzi wa minara katika maeneo hayo.

Naye Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi wa KINAPA Angela Nyaki amesema kuwa wapo tayari kushirikiana na watoa huduma katika kufanikisha upatikanaji wa huduma ya mawasiliano katika maeneo ya hifadhi kwa kuharakisha mchakato wa kutoa vibali sambamba na kuwapa watoa huduma maeneo ambayo wanaweza kujenga minara ya mawasiliano bila kuathiri uoto wa asili au viumbe hai vilivyopo katika hifadhi hiyo.

Ameongeza kuwa watalii wengi wanaofika mahali hapo kwa ajili ya kupanda Mlima Kilimanjaro wamekuwa wakishindwa kutumia huduma ya live streaming wakiwa juu ya mlima kutokana na mwingiliano wa mawasiliano na mtandao wa Safaricom wa nchini Kenya kitu kinachosababisha watalii kukosa mawasiliano wanapopanda mlima kwasababu simu zao zinakuwa zinasoma mtandao wa nchi jirani.

Kwa upande wa Afisa Uendeshaji wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Albert Richard amesema kumekuwa na malalamiko mengi ya watoa huduma kuhusu ucheleweshaji wa vibali vya ujenzi wa minara ya mawasiliano katika maeneo ya hifadhi za Taifa nchini kitu ambacho kinachangia kwa kiasi kikubwa kwa watoa huduma kuamua kwenda kujenga mnara katika maeneo ambayo hayana changamoto za utoaji wa vibali.

Aidha, watendaji wa TCRA, UCSAF, KINAPA pamoja na wawakilishi wa Makampuni ya simu nchini wamekiri kupokea maelekezo ya Naibu Waziri na kuahidi kuyafanyia kazi kama alivyoelekeza kwa lengo la kutatua changamoto ya mwingiliano wa mawasiliano katika maeneo ya mipakani na maeneo ya hifadhi za Taifa nchini.

Katika ziara hiyo Mhandisi Kundo aliambatana na watendaji kutoka katika taasisi za mawasiliano ambazo ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL),Shirika la Posta Tanzania (TPC) na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) pamoja na wawakilishi wa makampuni ya simu ya Vodacom, Tigo, Airtel, TTCL, Halotel na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Hai kwa lengo la kukagua ujenzi, ubora, uwezo na upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika maeneo ya mipakani.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Comments

Popular posts from this blog

Mkuu wa Mkoa wa Katavi akibidhiwa Ofisi,aelezwa Miradi ya kusimamia.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi Bi,Mwanamvua Hoza Mrindoko wa kwanza Kushoto akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Zuberi Homera wakati wa makabidhiano ya Ofisi. Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Katavi Beda Katani. Wakuu wa Wilaya,Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Jamila Yusuf na Mkuu wa Wilaya ya Mlele Rachel Kasanda. Na Mwandishi Wetu,Site Tv Mapema leo Mei 25,2021 Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Hoza Mrindoko,amekabidhiwa Ofisi na aliye kuwa Mkuu wa Mkoa huo Juma Zuberi Homera aliye hamishiwa Mkoani Mbeya kuwa Mkuu wa Mkoa. Katika makabidhiano hayo,Homera amemtajia Mkuu wa Mkoa wa Katavi miradi ambayo inatakiwa kusimamiwa hadi ikamilike ni pamoja na Bandari ya Karema,Hosipitali ya Rufaa Mkoa,Kiwanda cha Nguo,Jengo la Utawala pamoja na Umeme wa Gridi ya Taifa. Aidha,amesema Katavi ni Nyumbani hivyo atatoa ushirikiano kwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi huku akiwakaribisha Viongozi na Wananchi kwa ujumla katika Mkoa wa Mbeya. "Kuna hili la Gridi ya Taifa ambalo linaendelea,kuna Kiwan...

Tabasamu hili kwa Wanafunzi,Nuru imewaka Juu yao/Mwekezaji afanya Jambo ...

Ajira Mpya Wakaribishwa Mlele, Full Kula Bata/Makubwa yaja