Kulia Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw. Daudi Kaali Akimkabidhi Mkataba wa Ujenzi wa Miundombinu katika Skimu ya Kilimo cha Umwagiliaji Madibila Bw. David Noble Mkurugenzi wa Kampuni ya Ukandarasi ya White City International.
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjyzglKdFWCHm9WaWjKCbUpb4enpRRGMYKF34ATi_4onZrDq5SQwCvx1EH2q9wm9i0mNmmdiS_vclT6QockeLzL8Oza7GdpxKeUhl5X5wZZoZgXDY-_NH8wrJllYCVXsm5iL4k1MFX5Cwg/w640-h540/2+Mkulima+Shabani+Sawasawa.jpg)
Na. Mwandishi Wetu –Mbarali,Mbeya.
Ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kilimo cha Umwagiliaji
katika skimu ya Madibila iliyopo katika Halmashauri ya Mbarali Mkoani Mbeya,
umeanza Rasmi kwa mkandarasi kukabidhiwa eneo la ujenzi wa mradi na mkataba kwa
utekelezaji wa mradi huo, ambao una lengo la kusimamia ustahimilivu wa
maliasili kwa ajili ya ukuaji wa utalii na shughuli mbadala za kiuchumi kusini
mwa Tanzania.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Daudi Kaale, amesema Tume hiyo ina jukumu kubwa ya kusimamia kilimo cha umwagiliaji nchini na kuhakikisha kwamba Skimu ya kilimo kama ya Madibila inafikia malengo yaliyokusudiwa.
“Uzoefu unaonesha kuwa
serikali imejenga skimu nyingi kwa gharama kubwa lakini baada ya muda
hazitekelezi kazi zake au majukumu kama ilivyokusudiwa, tija na uzalishaji kupungua
na hata mundombinu kuharibika.” Alisema Kaale.
Alisisistiza kuwa kuanzia sasa ni hazma ya Tume ya Taifa ya
Umwagiliaji kuhakikisha kuwa miundombinu yote inarejea katika hali yake ya kawaida
na kufanya kazi katika malengo yaliyokusudiwa, ili kuongeza pato la Taifa,
kuondoa umaskini na kuhakikisha ongezeko la ajira kwa wananchi.
Akiongea katika makababidhiano hayo msimamizi wa Mradi huo
kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Mhandisi Mkuu Ebenezer Kombe amesema, yeye
kama Msimamizi Mkuu, ana jukumu la kusimamia ubora, gharama halisi za ujenzi na
muda wa miezi 18 ambao umepangwa kwa kazi kukamilika.
Kwa upande wake Muwakilishi wa Mkandarasi kampuni ya wazawa White
City Internatinal, Bwana. David Noble amesema, wakulima watapata nafasi ya
kuendelea na shughuli zao za kilimo wakati ujenzi ukiendelea, na watajitahdi
kufanya kazi kwa kiwango na wakati.
Bw. Shabani Juma Sawasawa ni mkulima katika eneo hilo,
amesema kuwa, ujio wa mradi utakuwa na manufaa ya kuokoa upotevu wa maji baada
ya ujenzi wa mfereji wenye urefu wa kilikometa tatu kukamilika “Wakulima
tutanufaika na kutunza maji pamoja na kuyaruhusu yaende katika mto Ruaha Mkuu
kwa matumizi ya viumbe hai wengine, Maliasili na Mazingira.”Alisisitiza
Mradi huo wa REGROW ni Mradi wa usimamizi stahimilivu wa
maliasili kwa ajili ya ukuaji wa utalii na shughuli mbadala za kiuchumi kusini mwa
Tanzania, Mradi ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia kwa kushirikiana na
Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
MWISHO.
Comments
Post a Comment