
Na. Swaum Katambo



Katika makabidhiano ya Ofisi,aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Mlele Rachel Kasanda amemuomba Mkuu mpya wa Wilaya hiyo Filberto Sanga kusimamia vifaa vinavyotakiwa kuletwa kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa Hospitali za Wilaya zilizopo Mlele na Mpimbwe ili ziweze kufanya kazi vizuri pindi zitakapomalizika.
Kasanda amemuomba DC Sanga pia kusimamia kwa ukaribu ukamilishaji wa Ujenzi wa Kituo cha Afya Ilunde kilichopo Kata ya Ilunde Halmashari ya Wilaya ya Mlele kwakuwa kipo mbali na mjini hivyo kupelekea vifaa vya Ujenzi kutofika kwa kutosha na kwa wakati.
"Watu wa Ilunde wapo mbali na sisi,mvua ikianza kunyesha wanawake wajawazito wanapata Changamoto kidogo ya mawasiliano kufika kwa wakati,nikuombe tuu kifuatilie kile kituo kwa ukaribu,ukifanyie kazi mpaka masika yanaanza wale kinamama na watu waliopo kwenye ile Kata waweze kupata huduma ya kutosha"Alisema Kasanda
Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Mlele Rachel Kasanda akimuomba Mkuu mpya wa Wilaya hiyo Filberto Sanga kusimamia utekelezaji wa Miradi inayoendelea
Kadhalika,amemuomba DC Sanga kufuatilia kwa ukaribu ukamilishaji wa Miradi mbalimbali inayoendelea kujengwa ikiwemo Miradi ya Nyumba za Wakuu wa Idara Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe,Ofisi za Wakurugenzi,Miradi ya Elimu ikiwemo na Madawati na kusema kuwa yupo tayari kumpa ushirikiano endapo kuna mahali kutamtatiza.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mlele Filberto Sanga mara baada ya kukabidhiwa Ofisi ameahidi kuyafanyia kazi yote aliyoshauriwa na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo Rachel Kasanda na kuiomba timu yote iliyofanya kazi na mtangulizi wake kuendelea kumpa ushirikiano.
Mkuu wa Wilaya ya Mlele Mhe.Filberto Sanga
Nae Lucas Kifyasi Mwakilishi wa Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mlele kwa niaba ya Wakurugenzi wote (Mlele na Mpimbwe) amemshukuru aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo Rachel Kasanda kwa ushirikiano alioutoa kwao huku wakiahidi kutoa ushirikiano kwa DC Sanga kwa kufanya vizuri kiutendaji na katika ukusanyaji wa Mapato ya ndani.

Lucas Kifyasi Mwakilishi wa Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mlele
Comments
Post a Comment