TAKUKURU KATAVI YAREJESHA FURAHA KWA HALMASHAURI, WAGONJWA,WAKULIMA MAFUNDI NA VIBARUA, ZAIDI YA TSH MIL 157,000,000/- ZAOKOLEWA
Na. Swaum Katambo
Mpanda-Katavi
TAKUKURU Mkoa wa Katavi inafanya uchunguzi kwa wahudumu wa Afya watatu katika Kituo cha Afya cha Ilembo kilichopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi kwa makosa ya wizi wa dawa za serikali na kuomba kupokea Rushwa kutoka kwa wagonjwa waliokuwa wamelazwa katika kituo hicho cha Afya.
Akitoa taarifa mbele ya waandishi wa Habari leo Disemba 19 Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Katavi Ndg.Christopher Nakua amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Hussein Hassan Kimaro,Charles Daniel na Isack Muhigi.
Hata hivyo amebainisha kuwa Mtuhumiwa Hussein Hassan Kimaro ambaye ni Muuguzi kwenye wodi ya wazazi katika kituo cha Afya Ilembo mnamo Desemba 14,2020 alikamatwa na begi likiwa na dawa mbalimbali za binadamu zikiwemo za Serikali na nyinginezo ambazo ilibainika kuwa alikuwa akiwauzia wagonjwa kwenye wodi ya wazazi hasa nyakati za usiku na baada ya kukamatwa alihojiwa na kukiri kutenda kosa hilo lakini alikimbia kwa lengo la kutaka kutoroka na pikipiki yake ambayo hakufanikiwa kuichukua.
Mtuhumiwa wa pili Charles Daniel pia ni muuguzi katika kituo hicho kwenye wodi ya wazazi alibainika kuomba Rushwa kwa mume wa mgonjwa aliyekuwa amelazwa kwenye kituo hicho cha Afya mnamo Desemba 13,2020 majira ya saa mbili usiku kiasi cha sh20,000/- lakini alipewa sh 10,000/- na mume wa mgonjwa huyo ili amsaidie mgonjwa wake kujifungua salama.
"Uchunguzi wa awali umeonesha kuwa baada ya ya muuguzi huyo kubanwa na muuguzi mfawidhi na Kaimu Mganga Mkuu wa Kituo hicho cha Afya alirudisha fedha hizo sh 10,000/- kwa muhusika"Alisema Nakua
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Katavi Ndg.Christopher Nakua Akitoa taarifa mbele ya waandishi wa HabariAidha Nakua alisema mtuhumiwa watatu ambaye Isack Muhigi ambaye pia ni muuguzi kwenye kituo hicho cha Afya mnamo Desemba 13,2020 majira ya mchana alimuomba mgonjwa na kupokea Rushwa ya kiasi cha sh 10,000/- ili amsaidie mgonjwa huyo kupatiwa huduma ya kujifungua salama,huku kesho yake mtuhumiwa hiyo baada ya kubanwa na Muuguzi Mfawidhi katika wodi hiyo ya wazazi alimrudishia mgonjwa huyo fedha zake mbele ya Kaimu Mganga Mkuu wa Kituo hicho cha Afya.
"Tunatoa wito kwa watumishi wa Umma Mkoani Katavi na jamii kwa ujumla kutojihusisha na vitendo vya kijinai kama kuomba na kupokea Rushwa au kuiba vifaa vya Serikali kwa sababu zozote zile" aliongeza
TAKUKURU Mkoa wa Katavi inaendelea na uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili wauguzi hao na pindi uchunguzi huo utakapokamilika na tuhuma hizo kuthibitika watuhumiwa watafikishwa Mahakamani.
Katika hatua nyingine TAKUKURU Mkoa wa Katavi kupitia ofisi ya TAKUKURU Wilaya Tanganyika katika kipindi cha Agosti hadi Desemba 2020 imefanikiwa kudhibiti fedha kiasi cha Sh Mil 136,757,060 fedha zilizokusanywa na wakusanya ushuru wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika huku kipindi cha mwezi Desemba pekee fedha zilizodhibitiwa ni sh 27,572,210.
Halmashauri hiyo tangu mwaka 2017 imekuwa ikiwatumia mawakala wa kukusanya Ushuru kutoka katika vyanzo vyake kama minada na vizuizi vya mazao, ambapo mikataba yao iliwataka wazabuni kukusanya ushuru kwa kutumia mashine za kielektroniki kwa mlipa ushuru kwa kila ushuru anaotoza.
Aidha anatakiwa kuweka kiasi chote anachokusanya kwenye akaunti ya Halmashauri ambapo ni MDC OWNSOURCE COLLECTION A/C yenye namba 61910000767 na wakala atalipwa 30% baada ya kuweka fedha hizo kwenye akaunti ya Halmashauri lakini baadhi ya mawakala walikiuka mikataba yao hawakuwasilisha fedha na hata walipopelekwa Mahakamani na kushindwa kesi hizo hawakuwasilisha fedha hizo.
"TAKUKURU Mkoa wa Katavi inawataka mawakala wote ambao ni wadeni sugu kuwasilisha fedha wanazodaiwa ndani ya siku 30 kianzia leo (Dec 19,2020) vinginevyo hatua kali zitachukuliwa" alisema Nakua Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Katavi.
Pia amewasihi mawakala na wakusanya ushuru wote katika Mkoa wa Katavi kufanya kazi zao kwa uaminifu na uadilifu ili kuongeza mapato ya Mkoa na Nchi kwa ujumla pia wananchi wote kulipa ushuru stahiki kila wanapotakiwa kufanya hivyo.
Katika tukio lingine pia TAKUKURU Mkoa wa Katavi kupitia ofisi yake ya Wialya ya Tanganyika imekuwa ikipokea taarifa za malalamiko kutoka kwa wananchi waliouza Pamba kupitia chama cha Msingi Kasekese (KASEKESE AMCOS) wakidai kutolipwa fedha zao za mauzo ya Pamba.
"Uchunguzi wa awali wa TAKUKURU wilaya ya Tanganyika umeonesha kuwa kulikuwa na upotevu mkubwa wa kilo 96,416 za Pamba yenye thamani ya sh 78,096,960 uliogundulika kutokana na tofauti ya Takwimu za kilo za Pamba zilizotolewa kwenye vituo vya ununuzi na kilo za Pamba zilizopokelewa kiwandani"Alisema Nakua
Makarani hao pia walikuwa wakiwasilisha majina yenye kilo hewa kiwandani mapema kabla ya wakulima wengine hivyo kurahisisha wizi huo na kuwafanya wengine kukosa malipo yao halali.
"Uchunguzi uliofanya na TAKUKURU umewezesha wadaiwa kufanya marejesho ambapo Desemba 15,2020 tumerejesha fedha za wakulima 11 ambazo ni jumla ya sh M 3,982,000 ambazo zilikwama kutokana na Changamoto mbalimbali za kibenki". aliongeza Nakua
Hata hivyo amesema awali wakulima 11 wa Pamba waliouzia katika kituo cha Kabage walilipwa sh Mil 9,636,570 kwa fedha ambazo ziliokolewa na TAKUKURU kutoka kwa makarani wa KASEKESE AMCOS huku uchunguzi na ufuatiliaji wa fedha zilizobaki unaendelea na mpaka sasa (Dec 19,2020) watu wawili wanashikiliwa kwa tuhuma mbalimbali kuhusiana na ubadhirifu huo.
"TAKUKURU Mkoa wa Katavi tunawataka watu wote waliohusika katika ubadhirifu huu hasa walio ingiziwa fedha tofauti na mauzo yao ya Pamba kujisalimisha na kutoa ushirikiano kabla ya kukamatwa na kushtakiwa,pia tunawasihi wananchi kwa ujumla kutoa ushirikiano ili kuwanasa watuhumiwa ambao wametoroka" aliongeza Mkuu wa TAKUKURU Katavi Christopher Nakua.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Tanganyika Romuli Rojas amewashukuru TAKUKURU kwa kutoa ushirikiano kwa uzito mkubwa pindi yanapotokea matukio mbalimbali katika Halmashauri hiyo na ametoa wito kwa makarani na vyama vya ushirika vitoe ushirikiano kwa wakusanyaji ushuru na wao kuwa waaminifu,pia amewataka watumishi wenzake kutojihusisha na kuhujumu mali za umma.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Tanganyika Romuli Rojas akiwashukuru TAKUKURU Mkoa wa Katavi Katika hatua nyingine pia Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Katavi Faustine Maijo amewasilisha taarifa inayohusisha ucheleweshaji wa malipo kwa makundi mbalimbali ambapo amesema mnamo Desemba 15,2020 walipokea malalamiko kutoka kwa mafundi na vibarua wa Kampuni ya MAMBA CONSTRUCTION inayojihusisha na utengenezaji wa barabara ya kutoka kwa Siwezi kwenda Kwalakwacha Manispaa ya Mpanda.
Alisema katika taarifa hiyo iliyowasilishwa na wawakilishi wawili ambao ni mafundi na vibarua waliotambulika kwa majina ya Samwel Majaliwa na Charles Mwenda walieleza kwamba toka mwezi Septemba mwaka huu vibarua hao hawakulipwa na Mkandarasi huyo hivyo kuwasababishia kuishi maisha magumu kiasi cha kukosa mwelekeo.
Waliamua kufika katika ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Katavi mnamo Dec 15,2020 ambao TAKUKURU ilifanikiwa kuwasiliana na Mkurugenzi wa Kampuni hiyo ya MAMBA CONSTRUCTION ambaye kwa maelekezo ya TAKUKURU alifanikiwa kurejesha baadhi ya pesa alizokuwa anadaiwa hivyo malipo kufanyika kwa vibarua na mafundi hao ambayo jumla yake ni kiasi cha sh Mil 8,772,000/- .
"Mnamo jana (Desemba 18,2020)Ndg Steven Kipingu ambaye ni Mhandisi wa Kampuni hiyo aliwasilisha TAKUKURU sh Mil 7,551,000 ambayo ni pungufu ya sh Mil 1,221,000 aliyoahidi kwa maandishi kuilipa baada ya kulipwa na mwajili wake TARURA na Tanroad"alisema Maijo
Pia Ndg.Maijo ametoa wito kwa Makandarasi na wote wanaopenda kudhulumu haki na stahiki za watu kuwa ni jambo baya ambalo linapelekea wizi kwa mafundi hao ili waweze kupata pesa za kujikimu.
Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Katavi Faustine Maijo amekiwasilisha taarifa yake mbele ya wanahabariKwa niaba ya Mafundi na vibarua wenzao baada ya kupokea pesa hizo Samwel Majaliwa na Charles Mwenda wameishukuru TAKUKURU Mkoa wa Katavi kwa kuwasaidia kupata malipo yao kwani walipitia Changamoto nyingi hususani za ugumu wa maisha kwani si wenyeji wa Mkoa wa Katavi bali ni wenyeji kutoka Mkoani Rukwa.
Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Katavi Faustine Maijo akiwakabidhi kiasi cha sh Mil 7,551,000 wawakilishi wawili wanaoidai Kampuni ya MAMBA CONSTRUCTION ambao ni Samwel Majaliwa na Charles Mwenda#SiteNews
#TukutaneSite
#TukutaneKazini





Comments
Post a Comment