CHAMA cha Ushirika cha msingi kimuli,kilichopo kijiji cha Utiri, kata ya Utiri
Wilayani Mbinga mkoani Ruvuma, kimetoa sh. milioni 100, kwa kwa ajili ya
kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika kata ya Kitanda, Utiri na
Kihangi mahuka.
Hayo yamesemwa na Meneja wa Chama hicho Ernest Komba, wakati
akisoma Taarifa ya utendaji kazi wa Chama hicho, Katika Ziara ya kukagua
Shughuli za Chama hicho cha Msingi iliyofanywa na Viongozi wa Chama
kikuu cha Ushirika Mbinga (MBIFACU) na viongozi wa ushirika ngazi ya
Mkoa wa Ruvuma.
Komba amesema kuwa fedha hizo zilizotolewa na Chama cha kimuli,
zilitokana na mapato ya premium na ziada, za Ndani na kusaidia ukarabati
wa majengo ya Taasisi za elimu na Afya, zilizomo katika maeneo
yanayohudumiwa na Chama cha kimuli.
Ameitaja miradi iliyopewa fedha na chama hicho kuwa ni Zahanati ya
Lipumba sh. milioni 14 ,Zahanati ya Kitanda milioni 9.5, Zahanati ya Utiri
milioni saba na Sekondari ya Ndela milioni 15.
Miradi mingine ni Sekondari ya Kihangi Mahuka milioni 13, Sekondari ya
Luli milioni 2.5, Sekondari ya Ngwilizi milioni 1 ,na Shule za Msingi 10
zilizoko katika Kata ya Utiri na Kitanda, ambazo zimepewa milioni 26.
Amesema awali wananchi walikuwa wakichangia fedha za mifukoni, au
kusubiri miradi itekelezwe na Serikali. Lakini kwa sasa Chama kimeona ni
vema kufanya maendeleo hayo ili kurudisha fadhila kwa wananchi ambao
huuza mazao katika chama cha msingi ambapo hivi sasa wananchi
wanaona faida ya uwepo wa chama cha Ushirika cha Msingi Kimuli.
“Chama kimetoa faida yake kwa kuchangia utekelezaji wa miradi
mbalimbali, ya Afya na elimu kwa kuchangia ukarabati na ujenzi wa
madarasa kutokana na uhitaji wa taasisi husika, ili kuamsha ari kwa jamii
na watambue umuhimu wa chama chao cha Ushirika, kwa kuwa kama sio
chama kutoa kiasi hicho basi wangelazimika kuchangia au kusubiri Serikali
itoe fedha za kutekeleza miradi hiyo ya Maendeleo”, Alisema Komba.
Kahawa ya kisasa katika shamba darasa la Kimuli AMCOS wilayani Mbinga
Komba ametoa rai kwa Wananchi wa kata zilizo katika mradi, huo
wajiunge na Chama cha ushirika na Msingi Kimuli kwa Maendeleo ya kaya
na Jamii kwa ujumla.
Licha ya kuchangia miradi ya maendeleo,Meneja huyo amezitaja, huduma
zingine zinazotolewa kuwa ni mradi wa Mashine ya kusaga nafaka ambao
hutoa huduma kwa wanachama, lengo likiwa ni kupata uzoefu na kupata
uzoefu wa kuanzisha kiwanda cha kuchakata unga wa mahindi ambapo
hivi sasa chama kina mashine tatu katika Vijiji vya Utiri Mtama na Kitanda.
Kulingana na Meneja huyo Chama cha Ushirika cha Kimuli kimeanzisha
Mradi wa Mashamba ya miti ambapo mpaka sasa tayari wameshapanda
ekari 30 za miti katika kijiji cha Kitanda, mahande na Mtama lengo likiwa ni
kuwa ni kitega uchumi kitakachoongeza mapato katika chama hicho hapo
baadaye.
Ili kuhakikisha wakulima wa kahawa wanaongeza uzalishaji wa zao la
kahawa Komba amesema Chama kimekuza miche bora ya
kahawa(Compact) ili kukuza hali ya uzalishaji wa zao hilo ambapo Katika
Msimu huu Chama kimepanda miche ya kahawa 120,000.
Miche ya kisasa ya kahawa 120,000 ya AMCOS ya Kimuli wilayani Mbinga
Amesema miche hiyo imeoteshwa kitaluni na kuwauzia wakulima kwa bei
rahisi ili wakulima waweze kuzalisha Kahawa bora.Pia chama kina mradi
wa usafirishaji mizigo kwa kutumia magari ya Chama kwa lengo la
kusafirisha mbolea,kahawa na vifaa vya ujenzi, ili kuongeza pato la
Chama.
Kwa mujibu wa Komba,Chama hicho cha ushirika pia hukusanya Mazao ya
wanachama na ya wakulima wengine kuyachakata na kuyatafutia soko la
ndani na nje ya nchi ili kjuimarisha ushirika.
Kaimu Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika Wilaya za Mbinga na
Nyasa(MBIFACU) Henerck Ndimbo amempongeza Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania John Magufuli kwa kuviongezea nguvu vyama vya
Ushirika na Msingi kwa kuwa kwa sasa wakulima wengi mara baada ya
kupata Elimu ya Ushirika wanauza mazao yao kupitia vyama vya ushirika
na kupata manufaa mengi ikiwemo kusomesha watoto kununua pembejeo
na kukuza pato la familia.
Kwa upande wake Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa
Ruvuma Bumi Masuba amekipongeza MBIFACU kwa kusimamia vema
Vyama vya Msingi hali ambayo imewezesha kuimarisha ushirika kuanzia
vyama vya msingi ambapo ametoa rai kwa wananchi kuvitumia Vyama vya
Ushirika vya Msingi vilivyoko katika Maeneo yao.
Utayarishaji wa kahawa unaosimamiwa na Kimuli AMCOS wilayani Mbinga
Mkoa wa Ruvuma wenye wilaya tano na Halmashauri nane una jumla ya
vyama vya ushirika 296 kati ya hivyo Halmashauri ya Wilaya ya Songea
kuna vyama 31,Hamashauri ya Mbinga 81,Namtumbo 59,Nyasa
15,Manispaa ya Songea 24,Tunduru 48,Halmashauri ya Madaba 8 na
Halmashauri ya Mji Mbinga 27.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Comments
Post a Comment